Luke 3

1Sasa, katika mwaka wa kumi na tano wa utawala wa Kaisari Tiberia, wakati Pontio Pilato alikuwa gavana wa Uyahudi, Herode alikuwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, na Filipo ndugu yake alikuwa mkuu wa mkoa wa Iturea na Trakoniti, na Lisania alikuwa mkuu wa mkoa wa Abilene, 2na wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, Neno la Mungu lilimjia Yohana mwana wa Zakaria, jangwani.

3Alisafiri katika mkoa wote kuzunguka Mto Yordani, akihubiri ubatizo wa toba kwa ajili ya msamaha wa dhambi

4Kama ilivyoandikwa katika kitabu cha maneno ya Isaya nabii, “sauti ya mtu aliaye nyikani, “Itengenezeni tayari njia ya Bwana, yatengenezeni mapito yake yaliyoonyoka.

5Kila bonde litajazwa, kila mlima na kilima vitasawazishwa, barabara zilizopinda zitanyoshwa, na njia zilizoparaza zitalainishwa. 6Watu wote watauona wokovu wa Mungu.”

7Hivyo, Yohana akawaambia makutano makubwa ya watu waliomjia wapate kubatizwa na yeye, “Ninyi uzao wa nyoka wenye sumu, nani aliwaonya kuikimbia gadhabu inayokuja?

8Zaeni matunda yanayoedana na toba, na msianze kusema ndani yenu, “Tunaye Ibarahimu ambaye ni baba yetu; kwa sababu nawaambia ya kwamba, Mungu anaweza kumwinulia Ibrahimu watoto hata kutokana na mawe haya.

9Tayari shoka limeshawekwa kwenye mzizi wa miti. Hivyo, kila mti usiozaa matunda mema, hukatwa na kutupwa motoni.

10Kisha watu katika makutano walimuuliza wakisema, “Sasa tunatakiwa tufanyeje?” 11Alijibu na kuwaambia, “kama mtu ana kanzu mbili anatakiwa atoe kanzu moja kwa mwingine ambaye hana kabisa, na ambaye ana chakula na afanye vivyo hivyo.”

12Kisha baadhi ya watoza ushuru walikuja pia kubatizwa, na wakamwambia, “Mwalimu, tunatakiwa kufanya nini? 13Akawaambia, “Msikusanye fedha zaidi kuliko mnachotakiwa kukusanya.”

14Baadhi ya maaskari pia wakamuuliza wakisema, “Na sisi je? Tunatakiwa tufanye nini?” Akawambia, “Msichukue fedha kwa mtu yeyote kwa nguvu, na msimtuhumu mtu yeyote kwa uongo. Ridhikeni na mishahara yenu.”

15Sasa, kwa kuwa watu walikuwa na shauku ya kumngojea Kristo atakaye kuja, kila mmoja alikuwa anawaza moyoni mwake kuhusu Yohana kama yeye ndiye Kristo. 16Yohana akajibu kwa kuwaambia wote, “Mimi nawabatiza ninyi kwa maji, lakini kuna mmoja ajaye ambaye ana nguvu kuliko mimi, na sisitahili hata kufungua kamba za viatu vyake. Atawabatiza ninyi kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

17Pepeto lake liko mkononi mwake ili kusafisha vizuri uwanda wake wa kupepetea ngano na kuikusanya ngano ghalani mwake. Lakini, atayateketeza makapi kwa moto ambao hauwezi kuzimika.

18Kwa maonyo mengine mengi pia, alihubiri habari njema kwa watu. 19Yohana alimkemea pia Herode mkuu wa mkoa kwa kumuoa Herodia, mke wa ndugu yake na kwa maovu mengine mengi ambayo Herode alikuwa ameyatenda. 20Lakini baadaye Herode alifanya uovu mwingine mbaya sana. Alimfunga Yohana gerezani.

21Kisha ilitokea kwamba, wakati watu wote walipokuwa wakibatizwa na Yohana, naye Yesu alibatizwa pia. Wakati alipokuwa akiomba, mbingu zikafunguka. 22Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili kama njiwa, wakati huo huo sauti ikaja kutoka mbinguni ikisema, “Wewe ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa sana na wewe.”

23Sasa Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa na umri upatao miaka thelathini. Alikuwa ni mwana (kama ilivyotadhaniwa) wa Yusufu, mwana wa Eli, 24mwana wa Mathati, mwana wa Lawi, mwana wa Melki, mwana wa Yana, mwana wa Yusufu,

25mwana wa Matathia, mwana wa Amosi, mwana wa Nahumu, mwana wa Esli, mwana wa Nagai, 26mwana wa Maati, mwana wa Matathia, mwana wa Semeini, mwana wa Yusufu, mwana wa Yuda,

27mwana wa Yoanani, mwana wa Resa, mwana wa Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, mwana wa Neri, 28mwana wa Melki, mwana wa Adi, mwana wa Kosamu, mwana wa Elmadamu, mwana wa Eri, 29mwana wa Yoshua, mwana wa Eliezeri,, mwana wa Yorimu, mwana wa Matathi, mwana wa Lawi,

30mwana wa Simeoni, mwana wa Yuda, mwana wa Yusufu, mwana wa Yonamu, mwana wa Eliyakimu, 31mwana wa Melea, mwana wa Mena, mwana wa Matatha, mwana wa Nathani, mwana wa Daudi, 32mwana wa Yese, mwana wa Obedi, mwana wa Boazi, mwana wa Salmoni, mwana wa Nashoni,

33mwana wa Abinadabu, mwana wa Aramu, mwana wa Hesroni,, mwana wa Peresi, mwana wa Yuda, 34mwana wa Yakobo, mwana wa Isaka, mwana wa Ibrahimu, mwana wa Tera, mwana wa Nahori, 35mwana wa Seruig, mwana wa Ragau, mwana wa Pelegi, mwana wa Eberi, mwana wa Sala,

36mwana wa Kenani, mwana wa Arfaksadi, mwana wa Shemu, mwana wa Nuhu, mwana wa Lameki, 37mwana wa Methusela, mwana wa Henoko, mwana wa Yaredi, mwana Mahalalei, mwana wa Kenani, mwana wa Enoshi, mwana wa Sethi, mwana wa Adamu, mwana wa Mungu.

38

Copyright information for SwaULB